Njama za serikali ya Nigeria dhidi ya Sheikh Zakzaky
Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa serikali ya nchi hiyo inatekeleza njama za kumuua shahidi Sheikh Ibrahim Zakzaky kiongozi wa harakati hiyo.
Ibrahim Suleiman alisema hiyo jana kuwa serikali ya Nigeria mara kadhaa imepinga ombi la harakati hiyo na familia ya Sheikh Zakzaky la kumpeleka nje ya nchi kwa ajili ya matibabu licha ya hali ya mwanazuoni huyo kuwa mbaya. Mwakilishi huyo wa ngazi ya juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ameongeza kuwa upo uwezekano kuwa njama zinafanywa ili kumuua shahidi polepole Sheikh Zakzaky.
Mwanaharakati huyo wa Kiislamu wa Nigeria ameendelea kubainisha kuwa Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo ndiye kikwazo kikuu cha kutoachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky kwa sababu hazingatii utekelezaji wa sheria. Ibrahim Suleiman amepongeza pia jitihada zinazofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na marjaa wa Kishia nchini humo kuhusu suala la Sheih Zakzaky. Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na mkewe walitiwa mbaroni katika shambulizi lililofanywa Disemba 13 mwaka juzi na wanajeshi wa Nigeria katika Husseiniya iliyopo katika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo. Mamia ya waumini wa Kiislamu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky waliuliwa shahidi katika tukio hilo. Mahakama Kuu ya Nigeria tayari imeagiza kuachiwa huru kiongozi huyo wa kidini na mkewe, hata hivyo jeshi na serikali ya Nigeria haziko tayari kutekeleza amri hiyo.