Mwanamke Mualgeria ateuliwa kuwa mkuu wa kikosi cha MONUSCO DRC
Bi Leila Zerrougui raia wa Algeria ameteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa, mkuu wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, Antonio Guterres Katibu Mkuu wa umoja huo amemteua Leila Zerrougui mwenye umri wa miaka 61 kutoka Algeria kuwa mkuu wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Bi Leila Zerrougui anachukua nafasi ya Maman Sidikou kutoka Niger anayemaliza muda wake. Taarifa zaidi zinasema kuwa, Leila Zerrougui anatarajiwa kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake hayo mapya kuanzia Januri mwakani.
Bi Leila Zerrougui amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Umoja wa Mataifa na ana uzoefu wa takribani miaka 30 katika uwanja wa sheria za kimataifa na utoaji misaada kwa raia.
Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO kimekuwa nchini humo tangu mwaka 1999.
Raia na mashirika mbalimbali ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakikosoa utendaji wa kikosi hicho.
Aidha mbali na kukosolewa utendaji wao, askari wanaounda kikosi cha MONUSCO mara kadhaa wamekumbwa na kashfa za ngono na vitendo vya ubakaji.