Raia 114 wauawa mashariki mwa Kongo mwezi Juni
-
Waasi wa M23 na mauaji ya raia Mashariki mwa Kongo
Waasi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi uliopita waliwauwa watu wasiopungua 114 kuwatekanyara wengine 17. Haya yameelezwa Shirika la Ufuatiliaji Usalama la Kivu Security Tracker.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa matukio 247 ya kiusalama yalisajiliwa katika mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ikilinganishwa na matukio 305 mwezi Mei mwaka huu.
Kundi la waasi la M23 lilitajwa kuwa ndilo mhusika mkuu wa ghasia dhidi ya raia mashariki mwa Kongo.
Vitendo vya ukiukwaji wa haki vilivyofanywa na waasi wa M23 vilihusishwa na mashambulizi waliyofanya katika maeneo ya Masisi na Rutshuru mkoani Kivu Kaskazini, ambapo raia walioshukiwa kuunga mkono kundi la wanamgambo wanaounga mkono serikali la Wazalendo walishambuliwa.
Shirika hilo la Ufuatiliaji Hali ya Usalama huko Kivu limebainisha kuwa: Miili ya raia isiyopungua 48 ilipatikana huko Bibwe katika eneo la Masisi baada ya mashambulizi ya waasi wa M23.
Ripoti hiyo imeorodhesha mapigano ya silaha 115 mwezi Juni mwaka huu, ambapo 46 kati yake yalihusisha kundi la M23 sawa na karibu asilimia 40 ya mapigano yaliyoripotiwa.
Wakati huo huo, ripoti ya shirika la Kivu Security Tracker imeeleza kuwa waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) wameendelea kuwa tishio kubwa kwa raia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ripoti hiyo imefafanua kuwa kundi la ADF liliua raia 62na kuwatekanyara wengine 57 mwezi Juni mwaka huu.
Wakati huo huo ripoti ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa Kongo imekumbwa na mojawapo ya migogoro mirefu na tata zaidi duniani, ikiambatana na majanga makubwa ya kibinadamu na kusababisha watu milioni 7 kuyahama makazi yao.