UN yataka kufanyika uchunguzi kuhusu ghasia za karibuni nchini Kongo
Umoja wa Mataifa umetaka kufanyika uchunguzi kuhusu ghasia zilizoikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Disemba mwaka jana.
Jean Pierre Lacroix Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na oparesheni za wanajeshi wa kulinda amani amesisitiza juu ya ulazima wa kuanza uchunguzi kuhusu ghasia na utumiaji mabavu dhidi ya raia waliokuwa wakiandamana tarehe 31 Disemba mwaka jana na kuhukumiwa wahusika wa ghasia hizo na wale wote waliokiuka haki za binadamu. Lacroix aliyasema hayo jana akiwa Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa watu watano waliuawa kwenye ghasia hizo huko Kinshasa.
Katika maandamano hayo, waandamanaji walimtaka Rais Joseph Kabila atangaze kuwa hatashiriki katika uchaguzi wa rais na achukue hatua za kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika kama ilivyopangwa. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na oparesheni za wanajeshi wa kulinda amani ameashiria hali ya kutia wasiwasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kueleza kuwa njia pekee ya kuiondoa nchi hiyo katika hali ya mgogoro ni kufanyika mazungumzo na ametahadharisha kuhusu hatua yoyote ya kuchelewesha kufanyika uchaguzi wa rais huko Kongo.