Rais wa Malawi awataka wananchi kuombea mvua
Rais Peter Mutharika wa Malawi amewataka viongozi wa serikali kuliongoza taifa hilo katika maombi maalumu ya kuomba mvua, katika hali ambayo nchi hiyo inakabiliwa na ukame na uhaba wa chakula.
Katika taarifa, Mutharika amelitaka baraza la mawaziri na maafisa wote wa ngazi za juu serikalini kuongoza shughuli ya kuombea mvua katika misikiti na makanisa kuanzia Ijumaa hadi mwisho wa wiki hii.
Taarifa hiyo imesema: "Rais anawaomba wafuasi wa dini zote kufanya maombi kwa ajili ya mvua yenye manufaa na msimu wenye mavuno katika siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili."
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Malawi ambayo ilikuwa inasumbuliwa na mafuriko kutokana na mvua nyingi, ilitangaza maafa katika wilaya 20 baada ya uharibifu mkubwa wa mazao ya kilimo uliosababishwa na hujuma ya wadudu wanaoharibu mazao.

Wadudu hao ambao wamevamia nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini wameshambulia wilaya 20 kati ya wilaya zote 28 za Malawi na kuathiri maelfu ya hekari za mashamba ya kilimo, suala ambalo limeathiri usalama wa chakula nchini humo.
Malawi ambayo ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani inakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na uhaba wa mvua, na chakula chake kikuu ni mahindi.