Italia yataka kusaidiwa nchi za Kiafrika ili zitatue tatizo la uhajiri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39455-italia_yataka_kusaidiwa_nchi_za_kiafrika_ili_zitatue_tatizo_la_uhajiri
Waziri Mkuu wa Italia amesisitiza juu ya udharura wa kusaidiwa nchi za Kiafrika kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi tatizo la uhajiri linalozikabili nchi za bara hilo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 25, 2018 06:52 UTC
  • Italia yataka kusaidiwa nchi za Kiafrika ili zitatue tatizo la uhajiri

Waziri Mkuu wa Italia amesisitiza juu ya udharura wa kusaidiwa nchi za Kiafrika kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi tatizo la uhajiri linalozikabili nchi za bara hilo.

Paolo Gentiloni amesema hayo wakati alipohutubia Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaofanyika mjini Davos Uswisi na kueleza kwamba, kuna haja kwa nchi za Kiafrika kusaidiwa ili kustawisha uchumi wa nchi hizo. 

Waziri Mkuu wa Italia ameongeza kuwa, kuna ulazima wa kutokomezwa mitandao na magenge yanayojihusisha na utendaji jinai na kuzisaidia nchi za Kiafrika ili ziweze kudhibiti mipaka yao zenyewe na wakati huo huo kuanzisha mfumo mzuri wa kisheria kwa ajili ya kudhibiti wimbi la wahajiri.

Wahajiri wa Kiafrika wakiwa nchini Libya

Wimbi la wahajiri kutoka katika baadhi ya nchi za Kiafrika wamekuwa wakiingia nchini Italia wakitokea Libya na kuifanya nchi hiyo kama kituo chao cha kwanza kabla ya kuelekea katika nchi nyyingine za bara Ulaya kwa ajili ya kwenda kutafuta maisha.

Karibu wahajiri laki moja na elfu 12 waliingia nchini Italia kupitia maji ya Bahari ya Mediterenia mwaka uliopita wa 2017 na kutokea Italia kuelekea nchi nyingine za Ulaya. Wakati huo huo karibu wahajiri 2,400 walipoteza maisha yao katika kipindi hicho, wakati wakijaribu kuvuka bahari kuingia Ulaya.

Wimbi la wahajiri wanaoelekea barani Ulaya wakitokea kaskazini mwa Afrika limekuwa changamoto kubwa kwa Umoja wa Ulaya na hata kupelekea kuzuka mgawanyiko mkubwa baina ya nchi wanachama wa umoja huo.