IOM: Wahajiri 30 wa Kiafrika wamekufa maji katika pwani ya Yemen
Kwa akali wahajiri 30 wa Kiafrika wameripotiwa kufariki dunia baada ya kuzama maji katika pwani ya Yemen, wakati wakielekea Djibouti.
Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) imewanukuu mashuhuda wakisema kuwa, boti iliyokuwa imebeba wahajiri kupindukia ilizama baada ya wafanya magendo ya binadamu kuanza kuwafyatulia risasi wahamiaji hao wa Kiafrika baada ya kuibuka mzozo kati yao.
IOM imesema kuwa, boti hiyo iliyokuwa imebeba raia 101 wa Ethiopia na 51 wa Kisomali ilikuwa inaelekea Djibouti ikitokea wilaya ya al Buraiqa katika Ghuba ya Aden kabla ya kujiri tukio la ufyatulianaji risasi na kuzama boti siku ya Jumanne.
Taarifa ya shirika hilo la wahajiri la Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, mzozo huo uliibuka baada ya wafanya magendo ya binadamu waliokuwa wakiwapeleka wahajiri hao nchini Djibouti kuwaiwaitisha pesa kwa nguvu wakimbizi hao.
Joel Millman, msemaji wa IOM amesema zaidi ya watu 87,000 walihatarisha maisha yao katika safari hizo za baharini za kuogofya, wakijaribu kufika Yemen mwaka jana pekee.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) zaidi ya wakimbizi elfu tatu waliaga dunia mwaka jana wakijaribu kufika Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania, akthari ya wahajiri hao wakiwa ni raia wa nchi za Kiafrika ambao wanataraji kupata maisha mazuri na ajira huko barani Ulaya.