Raia wa Sudan Kusini waendelea kuikimbia nchi yao kutokana na machafuko
Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR ameelezea ongezeko la raia wa Sudan Kusini wanaokimbia nchi yao kuelekea nchi jirani ya Sudan.
Noriko Yoshida ameyasema hayo Jumatano ya jana katika kikao cha kujadili matatizo ya wakimbizi, kilichofanyika mjini Khartoum mji mkuu wa Sudan na kuongeza kwamba idadi ya wakimbizi wa Sudan Kusini ambao hadi sasa wanaendelea kuishi nchini Sudan imeongezeka na kufikia laki nane. Kwa upande wake, Hassabu Mohamed Abdalrahman, Makamu wa Rais wa Sudan ameelezea kufungamana nchi yake na ahadi ya kuwapokea wakimbizi hao sambamba na kuwaandalia mahitaji ya awali.
Mohamed Abdalrahman amesema kuwa, Umoja wa Mataifa na nchi wafadhili, zinatakiwa kutuma haraka misaada yao ya kifedha kwa ajili ya wakimbizi hao na nchi wenyeji. Tangu tarehe 15 Agosti 2016 ambapo raia wa Sudan Kusini walianza kukimbilia nchini Sudan, serikali ya Khartoum iliwasilisha ombi la kutaka msaada wa kifedha kwa ajili ya wakimbizi hao. Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Sudan, nchi hiyo ni mwenyeji wa wakimbizi milioni mbili kutoka mataifa ya Ethiopia, Eritrea, Somalia, Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, Yemen na Syria.