Feb 19, 2018 03:05 UTC
  • Nigeria yawaachia huru mamia ya washukiwa wa Boko Haram

Serikali ya Nigeria imewaachia huru mamia ya watu waliokuwa wakishukiwa kuwa wananchama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram kwa ukosefu wa ushahidi katika kesi zilizokuwa zikiwaandama.

Hayo yamesemwa jana Jumapili na Salihu Othman Isah, Msemaji wa Wizara ya Sheria ya nchi hiyo ambaye ameongeza kuwa, agizo la kuachiwa huru washukiwa 475 wa Boko Haram lililotolewa siku ya Ijumaa.

Amesema washukiwa hao watarejeshwa katika majimbo yao kwa ajili ya 'kurekebishwa tabia' kabla ya kukabidhiwa jamaa zao.

Wanachama wa Boko Haram

 

Takriban washukiwa 1,670 wa kundi la kigaidi la Boko Haram ambao wamekuwa wakishikiliwa katika kambi ya kijeshi ya Kainji katika jimbo la Niger Delta la magharibi mwa Nigeria, wamepitia mchakato kama huu wa kesi zao kusikilizwa kwa pamoja, baadhi yao wakiachiwa huru tangu Oktoba mwaka jana 2017.

Genge la Boko Haram lilianzisha mashambulizi nchini Nigeria mwaka 2009 kwa madai ya kupinga elimu za nchi za Magharibi. Zaidi ya raia 20 elfu wa Nigeria, Cameroon, Niger na Chad wameshapoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya genge hilo la kigaidi tangu wakati huo hadi hivi sasa na wengine zaidi ya milioni mbili wamekuwa wakimbizi.

Tags