Polisi ya Rwanda yaua wakimbizi wa Congo
Polisi ya Rwanda imeua idadi kadhaa ya wakimbiizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliokuwa wakifanya maandamano mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa.
Ripoti zinasema maafisa wa polisi ya Rwanda waliwafyatulia risasi karibu wakimbizi elfu 3 waliokuwa wakipinga hatua ya Umoja wa Mataifa ya kukata mgao wao wa misaada. Polisi ya Rwanda inasema imelazimika kutumia nguvu baada ya wakimbizi hao kuanza kurusha mawe dhidi ya askari usalama.
Msemaji wa Polisi ya Rwanda, Theos Badege amesema: Polisi imetumia gesi ya kutoa machozi kutawanya wakimbizi wanaokadiriwa kuwa elfu tatu baada ya kuanza kurusha mawe na vyuma. Badege Ameongeza kuwa, kwa bahati mbaya baadhi ya wakimbizi wameaga dunia na wengine wamejeruhiwa.
Wakimbizi hao wanasema polisi ya Rwanda ilitumia risasi hai kukabiliana nao, suala ambalo linakanushwa na maafisa usalama wa serikali ya Kigali.
Wakimbizi hao pia wanasema polisi wa Rwanda wameshambulia kambi ya wakimbizi ya Kiziba.
Wakimbizi wa Congo walikuwa wakiandamana jana Alkhamisi kupinga hatua ya Umoja wa Mataifa ya kukata mgao wao wa misaada ya kibinadamu.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa asilimia mbili tu ya bajeti yake ya mwaka huu ya misaada kwa wakimbizi walioko Rwanda ndiyo iliyodhaminiwa hadi hivi sasa.