Uganda yatumia mfumo wa Biometrics kuwasajili wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41125-uganda_yatumia_mfumo_wa_biometrics_kuwasajili_wakimbizi
Uganda inatumia mfumo wa usajili wa alama za vidole (Biometric) kuwasajili wakimbizi wanaozidi kumimnika nchini humo kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemopkrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 03, 2018 12:43 UTC
  • Uganda yatumia mfumo wa Biometrics kuwasajili wakimbizi

Uganda inatumia mfumo wa usajili wa alama za vidole (Biometric) kuwasajili wakimbizi wanaozidi kumimnika nchini humo kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemopkrasia ya Kongo.

Zoezi hili limeanza katika makazi ya wakimbizi ya Oruchinga yaliyoko kusini magharibi mwa nchi hiyo ambako kuna maelfu kadhaa ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Msemaji wa shirika la kuwahudumia wakimbizi la UNHCR, Babar Baloch, akizungumza na  waandishi habari mjini Geneva, amesema, lengo la zoezi hili litakaloendelea hadi Septemba mwaka huu wa 2018, ni kuisaidia serikali ya Uganda kurekebisha dosari zozote za takwimu kuhusu wakimbizi.

Wakimbizi wakiwa kambini

Amesema zoezi la hilo litahakikisha kuwa wakimbizi na waomba hifadhi  wanaonekana katika mfumo wa kuwasajili na hivyo kuisadia serikali ya Uganda kuwa na takwimu sahihi. Aidha amesema hatua hiyo itahakikisha kuwa  vifaa na huduma zinazotolewa na UNHCR na washirika wake zinawafika walengwa.

Ameongeza kuwa UNHCR ikifanya kazi bega kwa bega na washirika wake, imeongeza wafanyakazi wengine 400 kuweza kupanua eneo la kufanyia kazi  kwa makazi mengine  zaidi ya 30 ya wakimbizi.

UNHCR imetoa  msaada wa kiufundi kwa zoezi hilo ikiwemo programu (software) ya kusajili alama za vidole ambayo tayari imetumika  kuwasajili wakimbizi milioni 4.4 katika nchi 48 duniani.

Pia ameeleza kuwa Uganda ina wakimbizi zaidi ya milioni moja  na inaendelea na siasa zake za kuwakaribisha watu wote ambao wanatoroka mateso na migogoro nchini mwao. Miezi miwili ya mwanzo wa mwaka 2018 , Uganda imepokea wakimbizi wapya zaidi ya 50,000 kutoka mashariki mwa DRC wakitumia mitumbwi kuvuka ziwa Albert.