Ebola imeua watu 139, wengine 600 wameambukizwa DRC na Uganda
-
Kirusi cha Ebola
Takriban wagonjwa 600 sasa wanashukiwa kuwa na Ebola na vifo 139 vikishukiwa kusababishwa na ugonjwa huo hali inayoongeza hofu ya kuenea zaidi kwa mlipuko wa sasa wa Ebola.
Katika taarifa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO, imesema aina mpya ya Ebola ni ile ijulikanayo kama Bundibigyo na imeripotiwa kugunduliwa wiki hii mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini, ikiwemo katika miji ya Bunia na Goma, huku Uganda nayo ikithibitisha wagonjwa viwili katika mji mkuu Kampala, ikiwemo kifo kimoja cha msafiri aliyetoka DRC.
Akizungumza mjini Geneva Uswisi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ametangaza rasmi mlipuko huo kuwa Dharura ya Afya ya Umma ya Kimataifa (PHEIC), hatua ambayo amesema ni ya kipekee kutokana na ukubwa wa hatari iliyopo.
Dkt. Tedros amesema “Hii ni mara ya kwanza kwa Mkurugenzi Mkuu kutangaza Dharura ya Afya ya Umma ya Kimataifa kabla hata ya kuitisha kikao cha Kamati ya Dharura. Ameongeza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na “uhitaji wa hatua za haraka kuzuia maambukizi zaidi na vifo”.
WHO imeonya kuwa hali ya usalama katika jimbo la Ituri imezorota tangu mwishoni mwa mwaka 2025 huku zaidi ya watu 100,000 wakikimbia makazi yao katika miezi miwili iliyopita kutokana na mapigano.
Shirika hilo limesema mazingira hayo pamoja na shughuli nyingi za migodini na usafiri wa watu vinaongeza hatari ya kusambaa kwa virusi hivyo ndani na nje ya mipaka.
Mlipuko huu unasababishwa na aina ya Bundibugyo ya virusi vya Ebola, ambayo WHO imesema haina chanjo wala tiba iliyoidhinishwa hadi sasa, hali inayoongeza hofu ya athari kubwa zaidi ikiwa hatua kali hazitachukuliwa mapema.
Dkt. Tedros amesisitiza kuwa “Janga hili linasababishwa na virusi vya Bundibugyo, aina ya Ebola ambayo haina chanjo wala tiba iliyoidhinishwa.”
Hata hivyo WHO imesema bado kuna hatua muhimu zinazoweza kusaidia kudhibiti mlipuko huo, zikiwemo ufuatiliaji wa wagonjwa, kutenga walioambukizwa, kufuatilia waliokutana nao na kuongeza elimu kwa jamii.
WHO imesema ingawa hatari ya mlipuko huo duniani bado ni ndogo, kiwango cha hatari nchini DRC na ukanda wa Afrika Mashariki kinaendelea kuwa cha juu, na kuonya kuwa msaada wa haraka wa kimataifa unahitajika kuzuia ongezeko kubwa la maambukizi na vifo.