AU: Mamlaka za ndani Somalia ziimarishe vita dhidi ya al-Shabaab
Mjumbe wa ngazi za juu wa Umoja wa Afrika nchini Somalia ameyataka maeneo yenye mamlaka ya ndani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika yaimarishe makabiliano dhidi ya kundi la kigaidi na la kitakfiri la al-Shabaab.
Francisco Madeira, Mjumbe Maalumu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU nchini Somalia ametoa mwito huo katika mazungumzo yake na rais wa eneo lenye mamlaka ya ndani la HirShabelle, Mohammed Abdi Waare na kuongeza kuwa, kuna haja vikosi vya usalama katika majimbo yenye mamlaka ya ndani nchini Somalia kupiga jeki vita dhidi ya genge la kigaidi la al-Shabaab.
Amesema kuangamizwa kwa genge hilo kutaandaa mazingira ya kukabidhi kikamilifu majukumu ya usalama kwa vikosi vya usalama nchini Somalia, kutoka kwa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, Amisom.
Madeira ambaye ni mkuu wa Amisom amesema licha ya kufahamu fika changamoto zinazolikabili eneo la HirShabelle kwa kuwa ndilo jimbo changa zaidi nchini Somalia, lakini amesisitiza kuwa kuna haja majimbo matano yenye mamlaka ya ndani nchini humo kuhakikisha kuwa kuna uthabiti na uundwaji wa mfumo wa uongozi katika maeneo ambayo yamekombolewa na Amisom toka mikononi mwa al-Shabaab.
Licha ya kundi hilo kupoteza maeneo mengi lililokuwa likiyadhibiti mwaka 2015, lakini limekuwa likitekeleza mashambulizi ya kila mara dhidi ya viongozi, asasi za serikali, askari na hata raia wa kawaida wasio na hatia katika kona mbali mbali za Somalia.