Mugabe: Sikudhani kuwa Mnangagwa atanigeuka
Rais wa zamani wa Zimbabwe amesema kuwa hakufikiria kuwa rais wa sasa wa nchi hiyo, Emmerson Mnangagwa angemgeuka na kusimama dhidi yake na amelaani hatua ya Mnangagwa ya kumuondoa madarakani kwa njia ya mapinduzi.
Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 94 aliiongoza Zimbabwe tangu ilipopata uhuru mwaka 1980 hadi alipolazimika kuondoka madarakani Novemba mwaka jana.
Amesema: "Sikuwahi kufikiria hata siku moja kwamba Emmerson Mnangagwa niliyemlea na kumleta serikalini na ambaye niliokoa maisha yake akiwa gerezani alikotishiwa kunyongwa, kwamba siku moja angenigeuka."
Mugabe amesema aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi na kwamba Emmerson Mnangagwa ametwaa madaraka kwa njia isiyo halali.
Emmerson Mnangagwa, aliyekuwa makamu wa Rais wa Zimbabwe alifutwa kazi na Robert Mugabe na kwenda uhamishoni Afrika Kusini kabla ya kurejea nchini na kuchaguliwa na Bunge kuwa rais wa nchi hiyo.