UN yaitahadharisha EU kuhusu mgogoro mpya wa wakimbizi kutoka Afrika
Umoja wa Mataifa umezitahadharisha nchi za Umoja wa Ulaya kuhusu mgogoro mpya wa wakimbizi kutoka Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuia ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP), David Beasley amesema, kushindwa kundi la kigaidi la Daesh katika nchi za Iraq na Syria kumezidisha harakati za wanachama wa kundi hilo katika nchi za kusini mwa jangwa na Sahara na kuna uwezekano suala hilo likasababisha mgogoro mpya wa wakimbizi barani Ulaya.
Beasley amesema kuwa, wanachama wengi wa makundi ya kigaidi waliotoroka Syria wamekimbilia katika nchi za Afrika za chini ya jangwa la Sahara ambalo lina jamii ya watu milioni 500.
Mkurugenzi Mtendaji wa WFP ameongeza kuwa, kundi la Daesh sasa linashirikiana na makundi mengine yenye misimamo ya kuchupa mipaka na suala hilo linaweza kusababisha matatizo makubwa kupita kiasi katika eneo la chini ya jangwa la Sahara barani Afrika.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa, hali hiyo inaweza kusababisha mgogoro mkubwa zaidi wa wahajiri kuliko ule uliosababishwa na vita vya Syria.