Mgogoro wa kisiasa nchini Somalia waitia wasiwasi IGAD
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42256-mgogoro_wa_kisiasa_nchini_somalia_waitia_wasiwasi_igad
Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD imeeleza wasiwasi iliyonao juu ya kushtadi mgogoro wa kisiasa nchini Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 26, 2018 23:03 UTC
  • Mgogoro wa kisiasa nchini Somalia waitia wasiwasi IGAD

Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD imeeleza wasiwasi iliyonao juu ya kushtadi mgogoro wa kisiasa nchini Somalia.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumatatu, IGAD imesema mkwaruzano mkubwa unaoshuhudiwa hivi sasa miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika huenda ukasababisha kuporomoka kwa mafanikio yaliyopatikana kwa ajili ya kuinasua nchi hiyo kutoka kwenye kinamasi cha ukosefu wa usalama na uthabiti.

Taarifa ya jumuiya hiyo ya kieneo imeongeza kuwa, "Kukosekana uthabiti wa kisiasa nchini Somalia, kuyayatia katika hatari matunda yaliyopatikana ndani ya miezi 12 illiyopita, katika nyuga za usalama, siasa na uchumi."

Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki imeitaka Serikali ya Federali ya Somalia kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo, huku ikiwataka viongozi wafanye kazi bega kwa bega kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwaka 2020.

Waziri Mkuu wa Somalia, Hassan Ali Khaire

Katika siku za hivi karibuni, Somalia imeshuhudia malumbano makali baina ya Waziri Mkuu wanchi hiyo, Hassan Ali Khaire na Spika wa Bunge la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, Mohamed Osman Jawari.

Mgogoro huo ulianza mapema mwezi huu, baada ya wabunge zaidi ya 100 wanaoegemea upande wa Waziri Mkuu, kuwasilisha hoja bungeni ya kutaka kuenguliwa madarakani Spika wa bunge, kwa madai kuwa amekuwa kizingiti kwenye shughuli za bunge hilo.