Askari wa Kulinda Amani wa UN waondoka Liberia baada ya miaka 15
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Liberia UNMIL kimefunga rasmi mlango uliofunguliwa miaka 15 iliyopita.
Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha mafanikio ya kufungwa rasmi tarehe 30 Machi 2018 kwa mpango huo.
Antonio Guterres amewapongeza watu na serikali ya Liberia kwa dhamira yao ya kugeuza ukurasa wa machafuko na vita nchini humo kuwa amani. Pia ameipongeza serikali ya nchi hiyo kwa kuendelea na juhudi za kuhakikisha kunakuwa na amani na maendeleo endelevu Liberia.
Kwa upande wa UNMIL Katibu mkuu ameshukuru mchango mkubwa uliotoa kwa ushirikiano na wadau wengine hususan Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ambayo walinda amani wake waliweka msingi wa mpango wa UNMIL kuingia na kusaidia mchakato mzima wa amani Liberia.
Guterres ameshukuru na kupongeza kazi nzuri iliyofanywa na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia, wa sasa na waliotangulia, wafanyakazi wasio askari na raia waliofanya kazi na UNMIL.
Pia amewaenzi walinda amani 202 waliopoteza maisha yao wakati wa miaka karibu 15 ya kazi ya UNMIL Liberia.
Guterres ameihakikishia Liberia kwamba Umoja wa Mataifa na familia yake utaendelea kuisaidia serikali ya nchi hiyo katika utekelezaji wa mipango ya mabadiliko ili kuhakikisha amani iliyopatikana kwa kazi ngumu inadumu na nchi hiyo na watu wake wanasonga mbele kimaendeleo.
Rais mpya wa Liberia, George Weah pia alihudhuria sherehe hizo za kumalizika shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Itakumbukwa kuwa Liberia, ambayo ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kupata uhuru, ilikumbwa na vita vya ndani kuanzia mwaka 1989 hadi 2003 ambapo watu karibu robo milioni waliuawa. Umoja wa Mataifa ulituma kikosi cha kulinda amani nchini humo mwaka 2003 na hatimaye amani ya kudumu sasa imepatikana nchini humo.