Hali ya kiafya ya kiongozi wa harakati ya Kiislamu Nigeria si nzuri
Hali ya kiafya ya Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, IMN, Sheikh Ibrahim Zakzaky, si nzuri na anahitaji matibabu ya dharura.
Hayo yamedokezwa na Yusuf Hamza, mwanaharakati wa kisiasa wa Nigeria katika mazungumzo na Shirika la Habari la Tasnim. Ametahadahrisha kuwa hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky ni mbaya mno na kuwa kuna wasi wasi huenda akalemaa na kupoteza uwezo wa kutembea.
Mwanaharakati huyo wa kisiasa ameongeza kuwa, wameshawatahadharisha maafisa wa serikali ya Nigeria kuwa Sheikh Zakzaky ni mstari mwekundi kwa Waislamu wa Nigeria na katu hawatanyamaza kimya kuhusu dhulma anazotendewa mwanazuoni huyo.
Amesema hadi sasa wakuu wa serikali ya Nigeria hawajatoa pendekezo lolote kuhusu mpango wa kumuachilia huru Sheikh Zakzaky pamoja na kuwa mahakama ya nchi hiyo imeamuru kiongozi huyo wa Waislamu aachiliwe huru.
Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashktaka.
Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo na serikali ingali inaendeleza ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.