Kipindupindu chaua makumi ya wakimbizi Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42702-kipindupindu_chaua_makumi_ya_wakimbizi_uganda
Zaidi ya wakimbizi 40 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu katika kambi za wakimbizi zilizoko nchini Uganda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 05, 2018 23:18 UTC
  • Kipindupindu chaua makumi ya wakimbizi Uganda

Zaidi ya wakimbizi 40 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu katika kambi za wakimbizi zilizoko nchini Uganda.

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limeripoti kuwa, wimbi kubwa la wakimbizi limesababisha msongamano mkubwa katika mahospitali na hali mbaya katika kambi za wakimbizi na kuchochea zaidi ugonjwa wa kipindupindu ulioanza mwezi Februari.

Taarifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu imesema kuwa, mazingira machafu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maji safi ya kunywa vimechangia sana mlipuko wa ugonjwa huo wa kipindupindu ambao hadi sasa umesababisha vifo vya zaidi ya watu 40 katika kambi za wakimbizi za Kyangwali na Kyaka II huko magharibi mwa Uganda.

Limeongeza kuwa zaidi ya kesi elfu mbili za maambukizi ya kipindupindu pia zimeripotiwa na kwamba upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira ni miongoni mwa mahitaji ya haraka kwa wakimbizi wa Congo.

Makumi ya watu wamefariki dunia kutokana na kipindupindu Uganda

Shirika la Msalaba Mwekundu linakadiria kuwa wakimbizi 70 elfu wa Congo wamewasili nchini Uganda tangu mwanzoni mwa mwaka huu na kwamba asilimia 80 miongoni mwao ni wanawake na watoto.

Nchi jirani na maeneo ya mashariki mwa Congo DR zinasumbuliwa na wimbi kubwa la wakimbizi lililosababishwa na mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la nchi hiyo na makundi ya waasi hususan katika mkoa wa kaskazini mashariki wa Ituri.