Zarif awasili Brazil baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Senegal
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili nchini Brazil mapema leo Jumanne katika safari yake ya kiduru ya kuzitembelea nchi kadha za Afrika na Amerika ya Latini.
Mohammad Javad Zarif ameelekea Brazil baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Macky Sall wa Senegal jana Jumatatu.
Baada ya kufanya mazungumzo na Rais Sall, Zarif aliwaambia waandishi wa habari kuwa, "Nina furaha sana kuona maagizo yaliyotolewa na Rais wa Senegal yataleta mustakabali wenye mwangaza katika ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi za nchi mbili hizi."
Akiwa mjini Dakar hapo jana katika safari rasmi ya siku moja, Dakta Zarif alikutana na kufanya mazungumzo pia na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Senegal, akiwemo spika wa bunge la nchi hiyo ya Afrika.
Katika mazungumzo na mwenzake Sidiki Kaba na Spika Moustapha Niasse wa Senegal, Zarif alisema kwamba Iran imeazimia kustawisha zaidi ushirikiano wake na nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anatazamiwa kuitembelea pia nchi nyingine ya Amerika ya Latini ya Uruguay na nchi nyingine ya Afrika, Namibia.