Watu 257 wapoteza maisha katika ajali ya ndege nchini Algeria + Video
Televisheni ya serikali ya Algeria imetangaza kuwa, watu wasiopungua 257 wamepoteza maisha baada ya ndege ya kijeshi kuanguka katika uwanja wa ndege wa Boufarik, nje ya mji mkuu wa nchi hiyo, Algiers.
Kabla ya hapo baadhi ya maafisa wa Algeria walikuwa wametangaza habari ya kupoteza maisha watu 200 baada ya ndege moja ya kijeshi kuanguka nchini humo.
Televisheni ya al Hadath iliwanukuu maafisa hayo wa Algeria wakisema leo Jumatano kuwa, ndege ya kijeshi iliyoanguka karibu na uwanja wa ndege wa Boufarik kaskazini mwa nchi hiyo imeua watu 200.
Taarifa mbalimbali zinaendelea kutolewa kuhusu ajali hiyo. Kwa mfano afisa mmoja wa jeshi la Algeria amesema kuwa, watu wote waliokuwemo kwenye ndege hiyo iliyoanguka katika na uwanja wa ndege wa Boufarik wamepoteza maisha.
Shirika moja la habari limesema, ndege hiyo imeanguka muda mchache baada ya kuruka kutoka katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Boufarik. Duru za eneo hilo zimesema kuwa, ndege hiyo aina ya Ilyushin Il-76, ilikuwa na watu 200. Hata hivyo kama tulivyosema, televisheni ya serikali ya Algeria imesema waliokufa ni watu 257.
Televisheni ya Ennahar imemnukuu afisa mmoja wa chama tawala cha Algeria akisema kuwa, wanachama 26 wa chama cha ukombozi wa Polisario walikuwemo kwenye ndege hiyo. Mtandao wa habari wa kieneo wa Algerie24 umesema kuwa ndege hiyo ilikuwa inaelekea katika mji wa Bechar wa magharibi mwa Algeria.

Picha zilizosambazwa na ukurasa mmoja wa Intaneti wa Algeria zinaonesha kutokea moshi mkubwa baada ya ndege hiyo kuanguka.
Ajali ya ndege hiyo inahesabiwa kuwa mbaya zaidi tangu mwaka 2003 wakati ndege moja ya Algeria ilipoanguka mara baada ya kupaa kutoka katika uwanja wa ndege wa Tamanrasset na kuua watu 102.