Uganda yakanusha kama imekubali kutuma wanajeshi wake katika vita dhidi ya Yemen
Serikali ya Uganda imekadhibisha habari kwamba imekubali kutuma wanajeshi wake nchini Yemen.
Tovuti ya habari ya gazeti la Daily Monitor linalochapishwa nchini Uganda imeripoti leo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Henry Oryem Okello ametangaza kwamba serikali ya Kampala imekadhibisha habari iliyoripotiwa na tovuti ya habari ya Misri ya Arabi21 kwamba itatuma askari elfu nane wa jeshi lake nchini Yemen.
Tovuti ya habari ya Arabi21 iliripoti hapo kabla kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati umefanya mazungumzo na Uganda kuhusiana na kuanzisha tena operesheni za kijeshi nchini Yemen.
Hii ni katika hali ambayo hapo jana serikali ya Uganda ilikadhibisha ripoti hiyo na kueleza kwamba, hakuna mpango wala mazungumzo ya aina hiyo ambayo yamefanyika kati ya Uganda na Imarati.
Mnamo mwezi Machi mwaka 2015, Saudi Arabia, ikiungwa mkono na Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine kadhaa ilianzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen sambamba na kuiwekea mzingiro nchi hiyo masikini ya Kiarabu wa ardhini, baharini na angani.
Hadi sasa makumi ya maelfu ya Wayemeni wameuawa na kujeruhiwa na mamilioni ya wengine wamebaki bila makazi na kulazimika kuishi maisha ya ukimbizi ndani na nje ya nchi yao kutokana na moto wa vita uliowashwa na utawala wa Aal Saud.
Hata hivyo vikosi vya jeshi la Yemen vikishirikiana na vile vya harakati ya wananchi ya Ansarullah vinajibu mapigo kwa hujuma za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia kwa kuzishambulia kwa makombora ngome za utawala huo na mamluki wake ndani ya Yemen na katika ardhi ya Saudi Arabia.../