Askari wa UN watuhumiwa kuwabaka watoto Sudan Kusini
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kutoka Nepal wanatuhumiwa kuwabaka watoto wadogo nchini Sudan Kusini.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric ametaja jinai hizo za ubakaji kama uhaini, hususan vitendo vya kubakwa watoto wadogo katika nchi hiyo ya Kiafrika, lakini amesisitiza kuwa Nepal imekubali kutuma timu ya uchunguzi wa madai hayo.
Haijabainika ni lini na ni wanajeshi wangapi wa UN raia wa Nepal waliowabaka mabinti wadogo nchini Sudan Kusini lakini umoja huo ulipokea malalamiko hayo mnamo Aprili 13.
Mwezi Februari mwaka huu, wanajeshi 46 wa Kikoso cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) raia wa Ghana walirejeshwa nyumbani kutoka kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini, baada ya kukabiliwa na tuhuma za ubakaji.
Kikosi cha UNMISS kina askari wapatao 14,800 wa Kofia Buluu katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza Disemba mwaka 2013 vimeshasababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.