WHO yazindua oparesheni ya kuwapa chanjo watoto milioni mbili Afrika
Shirika la Afya Dunia WHO limesema operesheni kubwa kabisa ya kutoa chanjo ya ugonjwa wa kipindupindu barani Afrika imezinduliwa, ili kuwasaidia watu milioni mbili katika nchi tano za Afrika.
Chanjo hiyo ya kunywa itatolewa kwa watu nchini Zambia, Uganda, Malawi, Sudan Kusini na Nigeria. Chanjo hiyo inatarajiwa kutolewa kwa dozi mbili, dozi ya kwanza inatoa kinga kwa miezi sita, na dozi ya pili inatoa kinga kwa miaka mitano.
Mkurugenzi wa WHO barani Afrika Bw. Matshidiso Moeti amesema, katika kila majira ya masika na inaponyesha mvua kubwa, kipundupindu hutokea na kuleta janga kubwa barani Afrika. Hadi kufikia jana Mei 7, nchi 12 zimeripoti kuwa na maambukizi ya kipindupindu yanayoendelea.
Mkuu wa Kampuni ya Gavi inayotoa dawa za chanjo Dr. Seth Berkley amesema utoaji mkubwa wa chanjo kama wa sasa haujawahi kutokea.
Kipindupindu kwa Kiingereza cholera ni ugonjwa hatari unaosababishwa na bakteria hasa katika utumbo mwembamba. Bakteria hao ambao huitwa vibriocholerae huweza kusababisha kuhara sana na kutapika kupindukia pamoja na homa kali.
Maambukizi hutokea hasa kupitia maji au vyakula vilivyochafuliwa na wadudu kama vile nzi. Wadudu hao huweza kuchafua vyakula endapo vyakula hivyo vitaachwa wazi bila kufunikwa chombo chochote na kuvutia nzi hao kutua juu ya vyakula hivyo na kuacha bakteria wanaosababisha ugonjwa wa kipindupindu kwa mtu atakayekula chakula hicho.