May 10, 2018 02:26 UTC
  • UN: Itachukua miaka kadhaa kuliangamiza kikamilifu kundi la Boko Haram

Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la magharibi mwa Afrika ametangaza kuwa, licha ya kuweko mafanikio katika kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram, lakini itachukua miaka kadhaa ili kuliangamiza kikamilifu kundi hilo.

Muhammad bin Chambas, mjumbe maalumu wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa magharibi mwa Afrika na eneo la Sahel Afrika amesema hayo pambizoni mwa kikao cha kieneo kuhusu Ukanda wa Ziwa Chad kilichofanyika katika mji wa Maiduguri kaskazini mashariki mwa Nigeria na kusisitiza kwamba, kwa sasa Boko Haram imegeuka na kuwa, mtandao wa kimataifa wa ugaidi.

Amesisitiza kuwa, ili kuliangamiza kikamlifu kundi hilo la Boko Haram patahitajika miaka kadhaa ili kufikia lengo hilo.

Mkutano huo kuhusu eneo la Ziwa Chad linalojumuisha nchi za Nigeria, Chad, Niger na Cameroon pamoja na mambo mengine umejadili namna ya kukabiliana na mashambulio ya kigaidi ya Boko Haram.

Muhammad bin Chambas, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa magharibi mwa Afrika

Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

Tags