Mtoto wa Sheikh Zakzaky: Sina taarifa ya hali ya wazazi wangu
Mtoto wa kiume wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, hana taarifa zozote kuhusiana na hali ya baba, mama na kaka zake wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.
Muhammad Ibrahim Zakzaky amesisitiza kuwa, hadi sasa hana taarifa zozote kuhusiana na hali ya wazazi wake pamoja na ndugu zake.
Mwana huyo wa Sheikh Ibrahim Zakzaky amekosoa hatua za ukandamizaji na zisizo za kibinadamu zinazofanywa na jeshi na viongozi wa serikali ya Nigeria.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Jumanne ya juzi Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na mkewe walifikishwa katika Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna.
Kesi hiyo imeakhirishwa hadi Juni 21, na wawili hao wamerejeshwa mjini Abuja.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walijeruhiwa vibaya na kukamatwa katika shambulizi lililofanywa na jeshi la Nigeria tarehe 13 Disemba 2015 katika Husainia ya mji wa Zaria huko Kaduna, kaskazini mwa Nigeria. Mamia ya wafuasi wa Harakati ya Kiislamu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky waliuliwa shahidi katika uvamizi huo wa jeshi la Nigeria.
Licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kutoa amri ya kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe, lakini hadi hivi sasa jeshi na serikali ya nchi hiyo inaendelea kukaidi amri hiyo ya mahakama na kuendelea kuwashikilia wawili hao kinyume cha sheria.