Ethiopia yamwita nyumbani balozi wake mdogo kutoka Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44904-ethiopia_yamwita_nyumbani_balozi_wake_mdogo_kutoka_saudia
Vyombo vya habari vya nchi za Kiarabu vimetangaza kuwa, baada ya Ethiopia kumwita nyumbani balozi wake kutoka Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, imemwita nyumbani pia balozi wake mdogo aliyekuweko mjini Jeddah.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 24, 2018 02:55 UTC
  • Ethiopia yamwita nyumbani balozi wake mdogo kutoka Saudia

Vyombo vya habari vya nchi za Kiarabu vimetangaza kuwa, baada ya Ethiopia kumwita nyumbani balozi wake kutoka Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, imemwita nyumbani pia balozi wake mdogo aliyekuweko mjini Jeddah.

Televisheni ya al Jazeera imevinukuu vyombo hivyo vya habari vikisema kuwa, serikali ya Ethiopia iliamua kumwita nyumbani balozi wake kulalamikia hatua ya utawala wa kiukoo wa Saudia ya kuchelewa kumwachilia huru Mohammed Hussein al Amoudi, bilionea wa Saudia mwenye asili ya Ethiopia.

Hatua hiyo ya ghafla ilizusha hisia tofauti na zote zilisema kuwa kitendo cha Ethiopia cha kuwaita nyumbani balozi na balozi wake mdogo waliokuweko nchini Saudia kina uhusiano wa moja kwa moja na kukamatwa bilionea huyo mwenye asili ya Ethiopia. Hata hivyo wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia imekanusha madai hayo.

Mohammed Hussein al Amoudi, bilionea mwenye asili ya Ethiopia ambaye anashikilia katika korokoro za Saudia

 

Gazeti la Addiss Standard la mjini Addiss Ababa leo Alkhamisi limezinukuu duru za kuaminika za wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia zikisema kuwa, Amin Abdul Qader Barakat, balozi wa Ethiopia nchini Saudi Arabia na balozi wake mdogo aliyekuweko Jeddah wote wamepewa amri ya kurejea nyumbani.

Hatua hiyo ya Ethiopia imechukuliwa katika hali ambayo Alkhamisi iliyopita Abiy Ahmed Ali, waziri mkuu wa nchi hiyo alifanya ziara ya siku mbili nchini Saudia na kutaka kuachilia huru bilionea Mohammed Hussein al Amudi mwenye asili ya Ethiopia lakini inaonekana alishindwa kuwakinaisha viongozi wa Saudi kwani baadae ilitangazwa kuwa bilionea huyo hakuachiliwa huru.

Bilionea al Amoudi alikamatwa nchii Saudia mwezi Novemba mwaka jana na hadi hivi sasa anashikiliwa katika korokoro za nchi hiyo kwa madai ya kufanya ufisadi wa fedha.