Rais wa Somalia auzulu na kuteua maafisa wapya wa nyadhifa mbalimbali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47506-rais_wa_somalia_auzulu_na_kuteua_maafisa_wapya_wa_nyadhifa_mbalimbali
Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia amefanya mabadiliko mapya kwa kumteua mkuu mpya wa majeshi pamoja na mkuu wa idara ya upelelezi ya nchi hiyo.
(last modified 2026-04-28T05:09:17+00:00 )
Aug 17, 2018 11:01 UTC
  • Rais wa Somalia auzulu na kuteua maafisa wapya wa nyadhifa mbalimbali

Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia amefanya mabadiliko mapya kwa kumteua mkuu mpya wa majeshi pamoja na mkuu wa idara ya upelelezi ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa redio ya taifa ya Somalia Rais Abdullahi Mohamed amemteua  Taher Adam Elmi, kuwa Mkuu Mpya wa Majeshi na Fahad Yassin, kuwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Taifa. Kadhalika Rais wa Somalia amemteua Aminah Said, kuwa Mkuu wa Ofisi ya Rais. Hata hivyo redio ya taifa ya Somalia haijataja sababu ya uteuzi huo, ingawa wahisani wa kimataifa wameituhumu serikali ya Mogadishu kuwa na ufisadi na kutozingatia muundo wa jeshi la taifa.

Jeshi la Somalia

Somalia imekuwa ikishuhudia hali ya mchafukoge na ghasia tangu ilipoondolewa madarakani serikali ya Mohamed Siad Barre, rais wa zamani wa nchi hiyo ya pembe ya Afrika, yaani tangu mwanzoni mwa muongo wa 90 hadi leo. Kundi la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab lenye mafungamano na genge la al-Qaidah, limekuwa likidhibiti sehemu kadhaa za ardhi ya Somalia hususan katika maeneo ya vijijini ambapo hatua za jeshi la serikali kwa kushirikiana na askari wa Umoja wa Afrika AMISOM, kwa ajili ya kurejesha udhibiti wa maeneo hayo, bado hazijazaa matunda.