Idadi ya Wasomali waliofukuzwa makwao yaongezeka maradufu
Idadi ya Wasomali waliolazimika kukimbia makazi yao imeongezeka mwaka huu na maelfu miongoni mwao wamekuwa wakimbizi tena kutoka kwenye makazi yao ya muda walikokimbilia kutokana na vita, ukame na mafuriko.
Ripoti iliyotolewa na Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC) imesema miongoni mwa sababu kuu zinazowafanya Wasomali wakimbie makazi yao ni wamiliki wa ardhi kutaka maeneo hayo ya Mogadishu kwa ajili ya ujenzi, bila ya kutoa muhula na taarifa hapo kabla.
Ripoti hiyo imesema kuwa, zaidi ya Wasomali laki mbili wamelazimishwa kuhama makazi yao kuanzia Januari hadi mwezi Julai mwaka huu, idadi ambayo ni mara mbili zaidi ya ile iliyolazimika kuhama makazi yao mwaka jana katika kipindi kama hicho.
Baraza la Wakimbizi la Norway linalojihusisha na misaada ya kibinadamu limeitaka serikali ya Somalia kushughulikia tatizo hilo na wamikili wa ardhi na kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa watu waliofukuzwa katika makazi yao.
Idadi kubwa ya Wasomali hao walikuwa wamekimbilia maeneo ya mjini kutokana na majanga ya kimaumbile na machafuko yaliyotokea katika maeneo mengine ya Somalia.
Mwaka jana Umoja wa Mataifa ulikadiria kuwa zaidi ya nusu ya jamii nzima ya watu wa Somalia wanahitajia misaada ya kibinadamu.