Sisitizo la Rais wa China la kustawisha uhusiano na bara la Afrika
Rais wa China amesisitiza udharura wa kustawishwa ushirikiano wa pande zote kati ya Beijing na bara la Afrika.
Akihutubia katika ufunguzi wa Kongamano la Tatu la Ushirikiano wa China na Africa (Focac) mjini Beijing jana Jumatatu, Rais Xi Jinping aliashiria udharura wa kuimarishwa ushirikiano baina ya China na Afrika kwa manufaa ya pande mbili na kueleza kuwa China inaliunga mkono bara la Afrika katika pande zote na ina hamu ya kustawisha uhusiano na nchi za bara hilo. Xi Jinping aliongeza kuwa China itaendelea kuheshimu suala la kutoingilia masuala ya ndani ya nchi za Afrika katika kushirikiana na nchi hizo. Vilevile ameashiria kiasi cha dola bilioni 60 zilizotolewa na nchi hiyo kwa bara la Afrika na kueleza kuwa, fedha hizo zitatolewa kama misaada ya serikali, kwa ajili ya uwekezaji na kuzisaidia kifedha taasisi na mashirika mbalimbali katika kustawisha miundo mbinu barani Afrika. Rais wa China ameongeza kuwa, Beijing ina mpango wa kuanzisha mfuko wa ushirikiano wa amani na usalama kati ya China na Afrika ambao utasaidia pia kutoa misaada ya bure ya kijeshi kwa Umoja wa Afrika.
Bara la Afrika licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili, lakini katika miongoni ya hivi karibuni halikupewa mazingatio katika mahusiano na stratejia za kiuchumi za madola makubwa ulimwenguni ambayo yanafuatilia uchumi na biashara ya kimataifa kwa lengo la kujidhaminia malighafi muhimu zinazohitajika katika viwanda vyao na vilevile kuongezeka hisa zao katika masoko ya duniani.
Katika miaka ya karibuni China ikiwa nchi ya pili yenye uchumi mkubwa zaidi duniani imekuwa na mtazamo maalumu kwa suala la kushirikiana na bara la Afrika na kwa msingi huo imeamua kuanzisha jukwaa la ushirikiano kati ya Beijing na nchi za bara hilo ili kuweza kutambua kwa makini fursa za kiuchumi na uwekezaji katika nchi hizo na kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kijeshi na bara la Afrika. Wakati huo huo suala la kupatikana masoko mapya ya nje ni moiongoni mwa mambo yanayopewa umuhimu makhsusi katika udiplomasia wa kibiashara wa China hasa kwa kutilia maanani bidhaa nyingi zinazozalishwa na makampuni ya Kichina, na hapana shaka kuwa bara la Afrika lina nafasi muhimu katika stratejia hiyo.
Viongozi wa Beijing wanaamini kuwa, kupanua masoko yao ya uuzaji bidhaa katika nchi nyingine khususan katika nchi za Kiafrika ni miongoni mwa njia wanazoweza kutumia hasa baada ya kupungua uuzaji wa bidhaa za nchi hiyo huko Marekani kutokana na siasa za Rais Donald Trump wa nchi hiyo za kuzibana nchi nyingine. China pia inalihesabu bara la Afrika kuwa bara linaloweza kudhamini mahitaji yake ya kimsingi na malighafi inazohitajia katika sekta ya viwanda kwa muda mrefu na kwa bei nafuu.
Vilevile vyanzo vya nishati vya bara la Afrika vinatambuliwa na Beijing kuwa miongoni mwa njia za kudhamini mahitaji ya nishati ya China ambayo kutokana na kasi yake kubwa ya ustawi wa kiuchumi imekuwa miongoni mwa wanunuzi na watumiaji wakubwa wa nishati duniani. Kwa msingi huo na kupitia vikao na mikutano kama huu wa sasa na nchi za Kiafrika, China inatoa vishawishi mbalimbali vya kuzisha hamu ya nchi hizo ya kushirikiana zaidi na Beijing.
Hotuba ya Rais wa China huko Beijing kuhusu mipango ya nchi hiyo ya kutoa misaada ya bure ya kijeshi kwa nchi za Kiafrika inabainisha namna Beijing ilivyo tayari kutumia pesa nyingi barani humo, suala ambalo pia linapewa mazingatio na nchi za Afrika.