Al Shabab washambulia kituo cha polisi Kenya
Magaidi wameshambulia kituo cha polisi katika mpaka wa Kenya na Somalia na kupora gari la polisi na kombora moja.
Tukio hilo limejiri mapema alfajiri ya leo Jumapili katika mji wa Diif, Wajir Kusini katika Kaunti ya Wajir ambapo maafisa watatu wa polisi wamejeruhiwa.
Maafisa wa polisi na kijeshi wameanzisha msako dhidi ya magaidi hao ambao wanaaminika kuwa wafuasi wa kundi la Al Shabab.
Maafisa wa usalama waliokuwa katika eneo hilo wanasema kulikuwa na washambuliaji karibu 100 ambao walifyatua risasi kiholela katika kituo hicho kilichokuwa na askari 18.
Mapigano hayo yalianza saa tisa alfajiri na kuendelea kwa masaa mawili kabla ya magaidi kuo kuiba gari hilo la Land Cruiser walilotumia kubeba majeruhi wao.
Hili ndilo shambulizi la kwanza la magaidi nchini Kenya katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Katika kipindi hicho Jeshi la Kenya limetoa pigo kubwa kwa magaidi wa Al Shabab nchini Somalia .