Sep 07, 2018 14:21 UTC
  • Jeshi la Nigeria laua magaidi 14 wa kundi la Boko Haram

Magaidi 14 wa kundi la Boko Haram wameuawa kwenye operesheni iliyofanywa na jeshi la Nigeria jana katika kijiji cha Pulka, wilaya ya Gwoza, mkoani Borno kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Msemaji wa jeshi Nigeria, Texas Chukwu amesema, watu 21 waliotekwa nyara na wanamgambo wa kundi hilo wameokolewa. Amesema vikosi vya usalama vilifanya operesheni hiyo baada ya kupata taarifa kuwa magaidi wa Boko Haram wamefanya shambulizi la ghafla, ambapo walichoma moto gari moja ya abiria na kuteka baadhi ya wasafiri.

Mashambulio ya kundi hilo la magaidi wakufurishaji nchini Nigeria na katika baadhi ya nchi jirani yaliyoanza mwaka 2009, hadi sasa yameshasababisha watu zaidi elfu 20 kuuawa na wengine zaidi ya milioni mbili na laki sita kupoteza makazi na kulazimika kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi.

Juhudi za serikali ya Nigeria za kuliangamiza kundi hilo la kigaidi hadi sasa hazijapata mafanikio kamili licha ya kushirikiana na nchi za eneo hilo kukabiliana na wanamgambo hao wakufurishaji. 

Tags