Mapigano yashtadi Libya, waliouawa Tripoli wapindukia 96
Wizara ya Afya nchini Libya imetoa indhari juu ya kushadidi mapigano katika mji mkuu Tripoli, ambapo idadi ya waliouawa katika ghasia hizo imeongezeka na kufikia watu 96, wakiwemo raia.
Vyombo vya dola leo Ijumaa vimeripoti kuwa, mbali na watu 96 kuuawa katika mapigano hayo kufikia sasa, wengine 16 hawajulikani waliko huku 444 wakijeruhiwa.
Taarira ya Wizara ya Afya ya Libya imebainisha kuwa, familia 123 zimelazimika kuyahama makazi yao kutokana na kushtadi mapigano hayo yaliyoanza tangu Agosti 26.
Jana Alkhamisi pekee, watu 11 wakiwemo raia wanane waliuawa huku wengine 33 wakijeruhiwa kusini mwa mji mkuu Tripoli.
Ghassan Salamé, Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema kuwa makundi yanayovunja makubaliano ya kusitisha vita nchini humo yatawekewa vikwazo na Baraza la Usalama la umoja huo.
Amesema, vikwazo hivyo vya Umoja wa Mataifa ambavyo vitawasilishwa karibuni hivi vitawahusu makamanda kadhaa wa makundi yenye silaha.
Haya yanajiri licha ya jitihada za kimataifa za kutaka kuona mazingira ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo kufikia Disemba 10 mwaka huu yanaandaliwa.
Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa na hali ya mchafukoge tangu kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi kufuatia uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) mwaka 2011.