Al Shabab washambulia msafara wa Umoja wa Ulaya, watu 3 wauawa Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48510-al_shabab_washambulia_msafara_wa_umoja_wa_ulaya_watu_3_wauawa_mogadishu
Watu watatu wameuawa katika shambulizi la kujilipua kwa bomu lililofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi la al Shabab dhidi ya msafara wa Umoja wa Ulaya mjini Mogadishu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 01, 2018 11:07 UTC
  • Al Shabab washambulia msafara wa Umoja wa Ulaya, watu 3 wauawa Mogadishu

Watu watatu wameuawa katika shambulizi la kujilipua kwa bomu lililofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi la al Shabab dhidi ya msafara wa Umoja wa Ulaya mjini Mogadishu.

Shambulizi hilo limetokea mchana wa leo katika barabara ya eneo la viwanda katikati ya mji wa Mogadishu.

Wafanyakazi wa huduma za afya wamesema kuwa wamechukua maiti za raia wawili na ya mtu aliyetekeleza shambulizi hilo na kwamba wengine wanne wamejeruhiwa.

Wapiganaji wa kundi la al Shabab wametangaza kuwa ndio waliofanya shambulizi hilo dhidi ya msafara wa magari yaliyokuwa na na bendera za Italia na Umoja wa Ulaya.

Jeshi la Italia limetangaza kuwa msafara huo umeshambuliwa wakati ulipokuwa ukirejea Mogadishu baada ya kukamilisha operesheni ya kutoa mafunzo na kwamba hakuna mwanachama wao aliyeuawa au kujeruhiwa.

Msafara wa EU umeshambuliwa Mogadishu.

Wapiganaji wa kundi la al Shabab wamekuwa wakishambulia askari wa kikosi cha Umoja wa Afrika cha kulinda amani nchini Somalia, AMISOM na jeshi la Somalia. Umoja wa Ulaya ni miongoni mwa wafadhili wakuu wa operesheni hiyo ya kulinda amani nchini Somalia.