Oct 10, 2018 14:22 UTC
  • AU yawataka Wacameroon kuwa watulivu wakisubiri matokeo ya urais

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amewataka wanasiasa wa Cameroon kuwa watulivu na kujizuia kutoa matamshi ambayo yanaweza kushadidisha taharuki katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.

Moussa Faki Mahamat amesema AU inafuatiliwa kwa karibu matukio yanayojiri hivi sasa nchini Cameroon, huku wananchi wakisubiri kwa hamu na shauku kuu matokeo ya uchaguzi wa rais.

Amesema malalamiko yote yanayohusiana na uchaguzi wa rais wa Oktoba 7 yanayapaswa kushughulikiwa na vyombo husika vya sheria. 

Kauli ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika inakuja wakati huu ambapo kuna wasiwasi wa kutokea ghasia za baada ya uchaguzi katika nchi hiyo ya Kiafrika, baada ya mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha Movement for the Rebirth of Cameroon (MRC), Maurice Kamto kujitangaza mshindi wa uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita.

Mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha Movement for the Rebirth of Cameroon (MRC), Maurice Kamto

Paul Atanga, Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo amesema Baraza la Katiba ndicho chombo pekee cha sheria chenye mamlaka ya kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo, huku akitishia kumchukulia hatua kali za kisheria mwanasiasa huyo. Baraza hilo linapaswa kutangaza matokeo rasmi ndani ya siku 15 baada ya uchaguzi wenyewe kufanyika.

Baadhi ya vyama vya upinzani viliungana siku moja kabla ya uchaguzi huo ili kupambana na Rais Paul Biya mwenye umri wa miaka 85 na ambaye yuko madarakani kwa karibu miaka 36 sasa. 

Tags