Oct 23, 2018 03:01 UTC
  • Wagombea wenye chuki na Uislamu wameongezeka sana wakati wa urais wa Trump

Uchunguzi mpya ambao ripoti yake imetolewa hivi karibuni unaonesha kuwa, kadiri muda wa uchaguzi mdogo wa bunge la Marekani unavyokaribia ndivyo wagombea wenye chuki na Uislamu wanavyozidi kujitokeza.

Gazeti la The Guardian limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, ripoti ya uchunguzi huo inaonesha kuwa, chuki dhidi ya Uislamu zimeongezeka sana nchini Marekani tangu alipoingia madarakani Rais Donald Trump.

Taasisi ya Waungaji Mkono wa Waislamu nchini Marekani (Muslim Supporters Organization) imechunguza kampeni 80 za uchaguzi wa wagombea mbalimbali zilizoripotiwa kutumia maneno ya chuki dhidi ya Uislamu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kugundua kuwa kampeni zote hizo ni za wagombea wa chama cha Republican cha Donald Trump.

Chuki dhidi ya Uislamu zimeongezeka sana nchini Marekani baada ya kuingia madarakani Donald Trump

Uchunguzi huo umethibitisha kuwa, wagombea wengi wenye chuki za kidini, yaani asilimia 64 kati yao imma wamechaguliwa, au wamepasishwa kugombea au wanaungwa mkono na Donald Trump.

Thuluthi nzima ya wagombea hao wana misimamo mikali zaidi ikilinganishwa na wengine. Wagombea hao wenye misimamo mikali zaidi wanaendesha kampeni za kunyimwa Waislamu wa Marekani hata haki zao za kimsingi kabisa za kuishi.

Katika kipindi cha tangu kuingia madarakani Donald Trump huko Marekani, vitendo vya unyanyasaji, ukandamizaji na udhalilishaji dhidi ya Waislamu vimeongezeka sana.

Itakumbukwa kuwa uchaguzi mdogo wa bunge unatarajiwa kufanyika tarehe 6 mwezi ujao wa Novemba, 2018, nchini Marekani.

Tags