Oct 26, 2018 14:33 UTC
  • Maelfu waandamana Kongo DR kupinga mashine za kielektroniki za kura

Maelfu ya wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamefanya maandamano hii leo katika mji mkuu Kinshasa na miji mingine mikuu ya nchi hiyo wakitaka kutotumika mashine za kupiga kura kwa njia ya kielektroniki, huku wakisisitiza kuwa mashine hizo huenda zikapelekea kuibiwa kura.

Baadhi ya waandamanaji hao wamesikika wakisema kuwa, "Tutapambana hadi kufa. Mashine ya kupigia kura ni mashine ya kuiba kura."

Maafisa usalama wametumwa kwa wingi katika miji ya Goma, Bukavu na Bunia kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, eneo linaloaminika kuwa ni ngome ya upinzani, ili kudhibiti maandamano hayo.

Hata hivyo kinara wa chama cha upinzani cha  Union for Democracy and Social Progress party, Felix Tshisekedi ambaye pia anatazamiwa kugombea urais katika uchaguzi huo wa mwishoni mwa mwaka huu hajashiriki wala kuonekana kuunga mkono maandamano hayo.

Mashine za kupigia kura zilianza kuwasili mapema wiki hii nchini DRC zikitokea Korea Kusini

Makontena 180 yenye mashine hizo za kupigia kura kutoka Korea Kusini sasa yapo njiani baharini na yanatazamiwa kuwasili Kongo DR mwishoni mwa mwezi huu. Tayari makontena kadhaa yameshawasili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Rais Joseph Kabila wa Kongo anatarajiwa kuondoka madarakani baada ya kushika hatamu za uongozi kwa miaka 17 kutokana na kuakhirishwa kwa muda mrefu uchaguzi wa rais ambao mara hii umepangwa kufanyika Disemba 23.

Uchaguzi huo ambao ulipaswa kufanyika kabla ya kumalizika muhula wa urais wa Kabila mwaka 2016; umeakhirishwa mara kadhaa, jambo linalotia shaka iwapo utafanyika kweli mwishoni mwa mwaka huu au la. 

Tags