Watu zaidi ya 30 wauawa katika mashambulizi ya kigaidi Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49406-watu_zaidi_ya_30_wauawa_katika_mashambulizi_ya_kigaidi_mogadishu
Watu zaidi ya 30 wameuawa katika mashambulizi ya kigaidi yaliyolenga Hoteli ya Sahafi mjini Mogadishu ambayo hutumiwa zaidi na maafisa wa serikali ya Somalia.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 09, 2018 23:56 UTC
  • Watu zaidi ya 30 wauawa katika mashambulizi ya kigaidi Mogadishu

Watu zaidi ya 30 wameuawa katika mashambulizi ya kigaidi yaliyolenga Hoteli ya Sahafi mjini Mogadishu ambayo hutumiwa zaidi na maafisa wa serikali ya Somalia.

Ripoti zinasema magaidi kadhaa walishambulia hoteli hiyo iliyoko karibu na makao makuu ya Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai ya Somalia kwa magari kadhaa yaliyokuwa na mabomu na kuua makumi ya watu. 

Afisa wa Jeshi la Polisi ya Somalia, Mohamed Ahmed amesema jeshi hilo na walinzi wa Hoteli ya Sahafi walifanikiwa kuzima mashambulizi mwengine mawili ya kigaidi yaliyolenga hoteli hiyo na kuangamiza magaidi wasiopungua 6.

Ripoti zinasema mmiliki wa Hoteli ya Sahafi, Abdifatah Abdirashid na walinzi wake watatu ni miongoni mwa watu waliouawa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. 

Watu walioshuhudia wanasema vipande vya miili ya maiti waliouawa katika hujuma hiyo vilitapakaa huku na kule na kwamba makumi ya watu wamejeruhiwa. 

Hujuma hiyo imefuatiwa na mapigano makali ya ana kwa ana baina ya wanamgambo waliokuwa na silaha na askari usalama na inatazamiwa kuwa, idadi ya watu waliouawa huenda ikaongezeka. 

Makumi ya watu wameuawa katika hujuma ya kigaidi, Mogadishu.

Msemaji wa kundi la al Shabab, Abdiasisi Abu Musab amesema kundi hilo limelenga Hoteli ya Sahafi mjini Mogadishu kwa sababu ya uhusiano wake na serikali ya Somalia ambayo kundi hilo linataka kuiondoa madarakani. 

Mwaka 2015 kundi la kigaidi la al Shabab lilishambulia hoteli hiyo hiyo ya Sahafi na kuua wanasiasa na wabunge kadhaa wa Somalia.