UN: Waliotekeleza hujuma ya kigaidi Somalia wawajibishwe
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali shambulio la kigaidi la Novemba 9 mjini Mogadishu nchini Somalia ambalo limeua raia wengi wasio na hatia na kujeruhi makumi ya wengine.
Katika taarifa iliyotolewa kuhusu shambulio hilo, wanachama wa Baraza la Usalama wametoa rambirambi zao kwa familia za waathirika pamoja na watu na Serikali ya Somalia na kuwatakia afueni ya haraka wote waliojeruhiwa. Vilevile wamepongeza jinsi wafanyakazi ya huduma ya kwanza na serikali walivyoitikia kusaidia majeruhi na kushughulikia waliopoteza maisha katika shambulio hilo.
Kundi la kigaidi la Al Shabab limedai kuhusika na shambulio hilo lililoua takriban watu 53 na kujeruhi zaidi ya mia moja, wakati gari lililokuwa limejaa mabomu lilipolipuka nje ya hoteli moja mjini Mogadishu. Al Shabab wanaipinga serikali ya sasa nchini Somalia na mara kadhaa wamehusika katika mashambulizi ya kigaidi.

Wajumbe wa Baraza la Usalama pia wamesema kwamba ugaidi wa aina yoyote ile bado ni tisho kubwa kwa amani na usalama duniani na kusisitiza haja ya kuwachukulia hatua za kisheria wahusika, watayarishaji, wafadhili wa visa vya kigaidi na kuhimiza mataifa yote kutekeleza wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama, kushirikina vilivyo na serikali ya Somalia na pia maafisa wote husika katika jukumu hili.