Mkutano wa amani wa Libya wamalizika nchini Italia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49498-mkutano_wa_amani_wa_libya_wamalizika_nchini_italia
Mkutano wa siku mbili wa amani wa Libya ulimalizika jana usiku katika mji wa Palermo nchini Italia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 14, 2018 03:18 UTC
  • Mkutano wa amani wa Libya wamalizika nchini Italia

Mkutano wa siku mbili wa amani wa Libya ulimalizika jana usiku katika mji wa Palermo nchini Italia.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kumnukuu Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte, akisema kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuheshimu haki ya kujitawala Libya na kujiepusha na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Amesema, mustakbali wa Libya unatia matumaini na aliwaambia hadhirina kuwa, inabidi mkutano huo wa amani utumiwe kwa ajili ya kuunga mkono mapatano ya kusimamisha vita ya mjini Tripoli na kufanya juhudi za kutekeleza makubaliano hayo katika maeneo mengine yote ya Libya.

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte (katikati) akiunganisha mikono na mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, Fayez al Sarraj (Kushoto) na Mkuu wa Jeshi la Taifa la Libya, Khalifa Haftar, mjini Palermo, Italia. 

 

Mapatano ya kusimamisha vita mjini Tripoli, kuitishwa mkutano wa wananchi wote wa Libya na mpango wa kufufua uchumi wa nchi hiyo kupitia kuimarishwa taasisi muhimu kama vile Benki Kuu na Shirika la Taifa la Mafuta ni miongoni mwa ajenda kuu zilizojadiliwa kwenye mkutano huo.

Tangu mwaka 2011 wakati lilipoanza wimbi la kuungusha utawala wa Kanali Muammar Gaddafi hadi hivi sasa, Libya haijawahi kuwa na utulivu wa hata siku moja. Madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yaliivamia kijeshi nchi hiyo wakati wa kampeni hiyo na kuteketeza miundombinu yake na baadaye kuitelekeza huku silaha zikiwa zimetapakaa mikononi mwa makundi mengi hasimu ambayo kila moja linapigania kuwa na ushawishi zaidi nchini humo hadi leo hii.