Kikao cha Umoja wa Afrika na juhudi za kurekebisha muundo wake
Kikao cha dharura cha Umoja wa Afrika kimeanza huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia huku viongozi wa umoja huo wakifanya juhudi za kurekebisha muundo wake ili waweze kupata fursa zaidi za utatuzi wa pamoja na kuongeza ushirikiano wa nchi za bara hilo.
Mwanzoni mwa kikao hicho ambacho kimehudhuriwa na viongozi wa nchi 55 za Afrika, Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika sambamba na kuashiria kwamba mabadiliko na matukio yanayotokea hivi sasa barani Afrika na duniani kwa ujumla, yanatilia mkazo udharura wa kuharakishwa mpango wa kufanyiwa marekebisho muundo wa huo, ametoa pendekezo la kubanwa vipaumbele vya umoja huo katika masuala ya usalama, kisiasa, na ushirikiano wa kiuchumi. Kikao hicho kinafanyika katika hali ambayo suala la kufanyiwa marekebisho muundo wa Umoja wa Afrika lilitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 2016, ambapo Rais Paul Kagame alipewa jukumu la kuandaa utangulizi wa kufanyika mabadiliko hayo. Lengo muhimu zaidi la marekebisho hayo, ni kupunguza utegemezi wa kifedha wa umoja huo kwa asasi za kimataifa na pia kufanyika vikao vyenye kutoa maamuzi ya kutekelezeka kivitendo.
Ukweli ni kwamba, uingiliaji wa madola ya Magharibi barani Afrika ndiyo sababu iliyowafanya viongozi wengi wa bara hilo kufikiria njia za kupunguza utegemezi wa Afrika kwa nchi za Magharibi. Mbali na marekebisho ya muundo wa Umoja wa Afrika, utatuzi wa matatizo ya kiuchumi kupitia ushirikiano wa kieneo, ushirikiano wa kijeshi na kiusalama katika kupambana na makundi ya kigaidi na makundi yanayofanya magendo ya usafirishaji haramu wa binaadamu na madawa ya kulevya na kadhalika utatuzi wa migogoro ya kisiasa ndani ya baadhi ya nchi za bara hilo, ni mambo ambayo yanatarajiwa kufanyiwa kazi. Katika uwanja huo, Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania amesema: "Afrika inakabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama zikiwemo za ugaidi, vitendo vya utumiaji mabavu, makundi yenye kuchupa mipaka na biashara haramu ya madawa ya kulevya, ambapo yote hayo ni kikwazo katika ustawi. Kukabiliana na changamoto hizo, kunahitaji hatua za pamoja na ushirikiano wa nchi zote za bara hili." Mwisho wa kunukuu.
Ingawa kwa muda mrefu sasa viongozi wa Umoja wa Afrika wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kupunguza utegemezi wao kwa madola ya Magharibi na kutaka kutatua matatizo ya sasa kwa kuongeza ushirikiano wa kieneo na kuimarisha asasi za kieneo, lakini mazingira ya sasa ya nchi za bara hilo yanaonyesha kwamba, bado kuna njia ndefu kabla ya nchi hizo kufikia kujitegemea na kujitawala kikamilifu. Kuhusiana na suala hilo, Chukwuemeka Eze, mwanasiasa mkongwe wa nchini Ghana sambamba na kusisitizia umuhimu wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya viongozi na wananchi wa bara la Afrika anasema: "Ushirikiano wa viongozi na wananchi wa bara la Afrika utaandaa mazingira ya kupatikana mabadiliko makubwa ndani ya bara hili." Hivi sasa viongozi wa Umoja wa Afrika wamepiga hatua moja mbele ya kivitendo kwa ajili ya utekelezaji wa mabadiliko katika taasisi hiyo, na wanataraji kwamba ushirikiano wa wanachama wa AU utakuwa na nafasi chanya na athirifu kwa ajili ya umoja huo kupunguza utegemezi wa kifedha kwa asasi za kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama. Wakati huohuo wengi wana wasi wasi kwamba sambamba na kumalizika muda wa uenyekiti wa Rais Paul Kagame kwa Umoja wa Afrika Januari mwakani na kuchukuliwa nafasi yake na Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri, huenda marekebisho hayo yakasimama.