UN yaipongeza Uganda na Chad kwa kuwasomesha watoto wakimbizi
Umoja wa Mataifa umezipongeza serikali za Uganda na Chad kwa kuwasomesha watoto wakimbizi katika shule za taifa na kuwafanya wawe na utangamano.
Hayo yalisemwa jana na Manos Antoninis, Mkurugenzi wa Ripoti ya Tathmini ya Elimu Duniani ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambaye ameongeza kuwa, jitihada za nchi mbili hizo licha ya kuwa maskini ni za kupigiwa mfano.
Amesema uzoefu unaonesha kuwa, mchakato wa kuwafanya watoto hao wakimbizi watangamane na kuwa na maingiliano una umuhimu mkubwa sana kwa mustakabali wao.
Amesema mwaka jana 2017, watoto wakimbizi milioni 4 hawakuwa shuleni. Kwa maneno mengine ni kuwa watoto hao sio tu walikoseshwa haki yao ya kupata elimu, bali pia nchi wenyeji zilipoteza fursa ya kuwatangamanisha watoto wakimbizi kutoka jamii mbalimbali.
Mkurugenzi wa Ripoti ya Tathmini ya Elimu Duniani ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) amebainisha kuwa, kadri watoto hao wanavyozidi kutenganishwa, ndivyo wanavyozidi kuhisi kuwa ni wakimbizi na wageni katika maeneo waliko.
Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, mapigano, mauaji na jinai nyinginezo ziliwafanya watu milioni 68.5 kuwa wakimbizi mwaka jana 2017 katika maeneo tofauti duniani, aghalabu yao wakiwa wakimbizi katika nchi zao.