Nov 22, 2018 14:43 UTC
  • Watu 7 wauawa katika hujuma ya Boko Haram nchini Niger

Watu waliojizatiti kwa silaha wanaoaminika kuwa na mfungamano na genge la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram wameshambulia kampuni ya kuchimba visima vya maji ya Ufaransa ya Foraco kusini mashariki mwa Niger na kuua watu wasiopungua saba.

Ofisa wa serikali katika kijiji cha Toumour mkoani Diffa ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wafanyakazi sita wa kampuni hiyo waliuawa papo hapo katika hujuma hiyo ya leo Alkhamisi ya watu wanaoaminika kuwa wanachama wa Boko Haram, huku mwingine wa saba akiuawa kwa kukatwa kichwa nje kidogo ya kampuni hiyo.

Kampuni hiyo ya Foraco yenye makao yake mjini Marseille nchini Ufaransa ni ya tatu kwa ukubwa duniani, inayojishughulisha na uchimbaji wa visima vya maji na madini, na kwa sasa inaendeleza shughuli hizo katika nchi 22 duniani ikiwemo Niger.

Mkoa huo wa Diffa mara kwa mara umekuwa ukishambuliwa na magaidi wa Boko Haram ambao wana maficho yao katika nchi jirani ya Nigeria.

Wanachama wa Boko Haram

Miezi michache iliyopita, askari kumi wa Niger waliuawa katika hujuma ya Boko Haram katika mkoa huo ulioko kusini mashariki mwa nchi, karibu na mpaka na Nigeria.

Kundi hilo la wakufurishaji limekuwa likifanya mashambulizi ya kikatili katika nchi ya Nigeria na majirani zake Niger, Chad na Cameroon, mashambulio ambayo hadi hivi sasa yameshapelekea makumi ya maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hizo za Afrika Magharibi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Tags