Magaidi wa Al Shabab waua watu 10 katika hujuma mpya Somalia
Magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Shabab nchini Somalia wameshambulia kituo kimoja cha mafunzo ya Kiislamu kati mwa nchi hiyo na kumuua mhubiri na watu wengine tisa waliokuwa hapo.
Afisa mwandamizi wa polisi katika eneo la Galkayo amethibitisha kuwa magaidi wa Al Shabab wameua watu 10 wakiwemo vijana na wanawake katika hujuma hiyo ya mapema leo Jumatatu.
Amesema mapigano yangali yanaendelea baina ya maafisa wa usalama na magaidi wa Al Shabab na yamkini idadi ya walipoteza maisha ikaongezeka.
Walioshuhudia wanasema gaidi aliyekuwa akiendesha gari ambalo lilikuwa limesheheni mabomu aliligongesha katika jengo la kituo hicho cha Kiislamu na kulipuka na baada ya hapo magaidi wengine wakaanza kufyatua risasi kiholela.
Magaidi wa Al Shabab wametangaza kuhusika na hujuma hiyo. Katika shambulio jingine Jumamosi magaidi wa al Shabab walitekeleza shambulizi la kuvizia dhidi ya askari wa Jeshi la Somalia kusini mwa nchi hiyo na kuua askari 10.

Wapiganaji wa kundi la al-Shabab wamekuwa wakishambulia askari wa kikosi cha Umoja wa Afrika cha kulinda amani nchini Somalia, AMISOM , jeshi la Somalia na maeneo ya raia.
Wanajeshi wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.