Uchaguzi DRC: Felix Tshisekedi arejea ili kuanza kampeni zake za uchaguzi
Kiongozi wa chama kikongwe zaidi cha upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amerejea nchini humo kwa ajili ya kuanza kampeni za kuwania kiti cha urais katika uchaguzi wa mwezi ujao.
Felix Tshisekedi ni kiongozi wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) na aliidhinishwa kuwa mgombea wa urais wa pamoja baada ya mazungumzo kati yake na mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation) Vital Kamerhe.
Mwafaka kati ya wawili hao uliafikiwa jijini Nairobi mnamo 23 Novemba, na jana ndiyo mara yao ya kwanza kurejea DR Congo kwa ajili ya kuuanza rasmi kampeni za uchaguzi.
Ingawa Tshisekedi ananadiwa kama mgombea wa umoja wa wapinzani, si yeye pekee anayeungwa mkono na ubia wa vyama vya upinzani.
Vyama vya upinzani nchini humo vilikuwa vimekutana Geneva Uswisi na kumteua Martin Fayulu kuwa mgombea wa pamoja wa umoja wa vyama vya upinzani.

Bw Fayulu ni mbunge ambaye si maarufu sana kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kuchaguliwa kwake kulionekana kutowafurahisha Tshisekedi na Kamerhe ambao walijiondoa kutoka kwa makubaliano hayo siku moja baadaye. Katika muungano wa UDPS na UNC, Tshisekedi atagombea wadhifa wa rais naye Kamerhe anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu iwapo muungano wao utashinda urais.
Uchaguzi wa Rais katikka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umepangwa kufanyika tarehe 23 ya mwezi ujao wa Disemba ambapo chama tawala cha Rais Kabila pamoja na vyama vyake tanzu vimemteua Emmanuel Ramazani Shadary kuwania kiti cha urais.