Maandamano yafanyika Somalia kupinga kuvuliwa madaraka Rais Farmajo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50097-maandamano_yafanyika_somalia_kupinga_kuvuliwa_madaraka_rais_farmajo
Wafuasi wa Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa Somalia wamefanya maandamano katika mji mkuu Mogadishu, kupinga kitendo cha wabunge kuwasilisha hoja bungeni ya kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais huyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 11, 2018 04:38 UTC
  • Maandamano yafanyika Somalia kupinga kuvuliwa madaraka Rais Farmajo

Wafuasi wa Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa Somalia wamefanya maandamano katika mji mkuu Mogadishu, kupinga kitendo cha wabunge kuwasilisha hoja bungeni ya kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais huyo.

Baadhi ya watu walioshiriki maandamano hayo ya jana walisikika wakisema, "Hoja hiyo dhidi ya Rais Farmajo haina uhalali, kwa msingi kuwa Somalia haina Mahakama ya Katiba."

Wabunge wapatao 93 wanaotaka kuvuliwa madaraka Rais Farmajo siku ya Jumapili walimkabidhi Mohamed Mursal, Spika wa Bunge la nchi hoja hiyo, wakimtuhumu rais huyo kwa uhaini baada ya kusaini 'kisiri' makubaliano ya kisiasa na kiuchumi na Ethiopia na Eritrea.

Wakati huohuo, Abirahman Abdishakur Warsame, mkosoaji mkubwa wa serikali ya Mogadishu jana Jumatatu alirejea nchini  humo baada ya kuweko uhamishoni wa khiari kwa muda mrefu.

Rais Farmajo wa Somalia

Kiongozi huyo wa upinzani ambaye wakati mmoja alikuwa Waziri wa Mipango wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika amesema ataongoza maandamano ya amani mwezi huu mjini Mogadishu, kwa ajili ya kuwakumbuka walinzi wake watano waliouawa baada ya makazi yake kuvamiwa mnamo Disemba 17 mwaka jana. 

Mbali na changamoto za kisiasa, Somalia inakabiliwa na matatizo mengi kama ya ukosefu wa usalama kutokana na mashambulio ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabab pamoja na ukame ambao umeifanya nchi hiyo kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.