Dec 19, 2018 02:50 UTC
  • Jeshi la Cameroon laua wanachama 7 wa kundi linalotaka kujitenga

Jeshi la Cameroon limetangaza habari ya kuua wanachama saba wa waasi wa Ambazonia katika mji wa Bamenda, katika eneo lenye wazungumzaji wengi wa Kiingereza la kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Ofisa wa Afya katika mji huo amesema askari wanne wamejeruhiwa katika mapigano hayo mapya baina ya jeshi la Cameroon na waasi wanaotaka kujitenga. Jeshi la Cameroon halijasema iwapo askari wake wameuawa au kujeruhiwa katika makabiliano hayo.

Hata hivyo Jenerali Agha Robinson amesema wanajeshi wa nchi hiyo wanapata kibarua kigumu cha kupambana na wanachama wa kundi hilo la Ambazonia, kwa kuwa wanajificha miongoni mwa raia wa kawaida.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya wanachama 289 wa kundi hilo kuachiwa huru, baada ya Rais Paul Biya wa nchi hiyo kuwatangazia msamaha.

Mwezi uliopita, mapigano baina ya Jeshi la Cameroon na wapiganaji wa kundi hilo linalotaka kujitenga yalipelekea watu 15 kupoteza maisha katika eneo hilo la watu wanaozungumza Kiingereza katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Waasi wa Ambazonia

Wazungumzaji wa Kiingereza wanaunda karibu asilimia 20 ya wakazi wote milioni 20 wa Cameroon, nchi ambayo lugha yake rasmi ni Kifaransa. 

Kwa mujibu wa International Crisis Group (ICG), raia 500 na maafisa usalama 200 wameuawa tangu kundi hilo la Ambazonia lianzishe mashambulizi ya silaha dhidi ya askari usalama katika eneo hilo mwishoni mwa mwaka jana. 

Tags