AU yaitaka Burundi ipunguze askari wake Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50322-au_yaitaka_burundi_ipunguze_askari_wake_somalia
Umoja wa Afrika umeitaka Burundi ipunguze askari wake katika kikosi cha kulinda amani cha umoja huo, maarufu kama AMISOM, nchini Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 21, 2018 11:13 UTC
  • AU yaitaka Burundi ipunguze askari wake Somalia

Umoja wa Afrika umeitaka Burundi ipunguze askari wake katika kikosi cha kulinda amani cha umoja huo, maarufu kama AMISOM, nchini Somalia.

Umoja wa Afrika umewaandikia wakuu wa Burundi barua na kuwataka wapunguza askari 1000 walio katika kikosi cha nchi hiyo kinachohudumu katika fremu ya AMISOM nchini Somalia ifikapo Februari 28 mwakani.
Burundi ina idadi ya pili kwa ukubwa ya askari wa kulinda amani  katika kikosi cha AMISOM  ambapo ina wanajeshi 5,400, baada ya Uganda, ambayo ina askari 6,200. Nchi nyingine zenye askari katika kikosi cha AMISOM ni  Djibouti, Ethiopia na Kenya. Inasemekana kuwa uamuzi huo ni hatua jumla ya kupunguza askari wa AMISOM nchini Somalia. Hatua ya kuitaka Burundi ipunguze askari wake Somalia inakuja huku kukiwa na uhusiano mbaya baina ya Umoja wa Afrika na nchi hiyo.

Umoja wa Afrika umeikosoa vikali Burundi kutokana na rekodi yake mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu. Kuwepo askari wa Burundi katika kikosi cha AMISOM ni chanzo kikubwa cha fedha za kigeni kwa nchi hiyo ambayo imekuwa ikipokea dola milioni 18 kila miezi mitatu kutoka kwa AU kama malipo ya kushiriki katika kulinda amani Somalia. Wakuu wa Burundi hawajafurahishwa na uamuzi huo wa AU. Askari wa AMISOM wako nchini Somalia kurejesha amani na kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na magaidi wakufurishaji wa Al Shabab.