Israel inashirikiana na waasi kufanya magendo ya dhahabu Sudan
Imearifiwa kuwa utawala wa kizayuni wa Israel unashirikiana na makundi ya waasi nchini Sudan kufanya magendo ya dhahabu na madini ya urani katika jimbo la Kordofan Kusini.
Hassan Abadallah Dudu, chifu katika mtaa mmoja wa jimbo hilo amekiambia Kituo cha Habari nchini Sudan SMC kuwa, makampuni ya Israel yanashirikiana na waasi wa Harakati ya Ukombozi wa Sudan tawi la Kaskazini (SPLM-N) kufanya magendo ya madini hayo ya thamani na kuyapeleka katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Habari zaidi zinasema kuwa, mbali na dhahabu na urani, makampuni hayo ya utawala haramu wa Israel yanachimba madini mengine na kufyonza rasilimali katika wilaya ya Umm Sardaba, katika jimbo la Kordofan Kusini na kuzipeleka katika ardhi za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu.
Disemba mwaka 2014, ripoti ya Kituo cha Habari nchini Sudan ilibainisha kuwa, waasi wa SPLM wanatumia mapato ya biashara hiyo haramu kufadhili uasi wao dhidi ya serikali ya Khartoum.
Serikali ya Sudan imekuwa ikisisitiza kuwa, makundi hayo ya waasi yanafanya jinai za kutisha katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile kwa kuungwa mkono na serikali ya Juba.
Tangu mwaka 2003, Sudan imekuwa ikikabiliwa na uasi katika eneo la Darfur; huku harakati tofauti za uasi zikizuka huko Blue Nile na Kordofan Kusini tangu eneo la kusini mwa nchi hiyo lilipojitenga mwaka 2011 na kuunda nchi ya Sudan Kusini.