Vyama vikuu vya upinzani Sudan vyaafikiana kuunga mkono maandamano ya wananchi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50397-vyama_vikuu_vya_upinzani_sudan_vyaafikiana_kuunga_mkono_maandamano_ya_wananchi
Vyama vikuu vya upinzani nchini Sudan vimeafikiana kuunga mkono vuguvugu la maandamano ya wananchi katika miji mbalimbali wanaopinga hali mbaya ya kiuchumi na ughali wa maisha.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Dec 24, 2018 15:05 UTC
  • Vyama vikuu vya upinzani Sudan vyaafikiana kuunga mkono maandamano ya wananchi

Vyama vikuu vya upinzani nchini Sudan vimeafikiana kuunga mkono vuguvugu la maandamano ya wananchi katika miji mbalimbali wanaopinga hali mbaya ya kiuchumi na ughali wa maisha.

Makundi ya Muungano wa Nidaa Sudan na ule wa Mwafaka wa Kitaifa yalifanya mkutano jana kujadili jinsi ya kuunganisha pamoja nguvu za kambi ya upinzani na yameafikiana kuyaunga mkono maandamano yanayofanywa na wananchi wa Sudan tangu Jumatano iliyopita kupinga sera za kiuchumi za serikali ya Rais Omar al Bashir.

Wasudan katika majimbo 12 ya nchi hiyo wamekuwa wakifanya maandamano karibu kila siku wakipinga serikali na kutaka kutatuliwa matatizo yao mengi ya kiuchumi. Waandamanaji hao pia wanataka serikali ya Rais Omar al Bashir iondolewe madarakani kutokana na kushindwa kuendesha nchi.

Maandamano ya Wasudan wakipinga serikali ya Rais al Bashir

Serikali ya Sudan imetangaza hali ya hatari na amri ya kutotoka nje katika baadhi ya mikoa sambamba na kufunga mashule na vyuo vikuu vikiwemo vya mjini Khartoum.

Serikali inadai kuwa watu 8 wameshauawa hadi hivi sasa kwenye maandamano hayo lakini duru za kujitegemea na vyama vya upinzani vinasema kuwa waliouawa hadi sasa ni baina ya watu 22 hadi 28 huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.